Thursday, December 1, 2011

Tanga cement kuidhamini timu ya Taifa

KAMPUNI ya Saruji Tanga (Tanga Cement Ltd) imejitosa kupiga jeki maandalizi ya timu ya taifa ya tenisi itakayoshiriki michuano ya timu ya Davis Cup.

Timu hiyo ya taifa ya wachezaji kumi inatarajia kukaa kambini kwa wiki moja mjini Tanga kwa ajili ya maandalizi chini ya kocha Mtaliano Fabrizio Calderone.

Katibu Mkuu wa Chama cha Tenisi Tanzania (TTA) Inger Njau, alisema Dar es Salaam, kuwa kocha huyo anatarajia kuwasili nchini Desemba 11 kwa ajili ya kambi hiyo itakayoanza Desemba 14 hadi 21.

Inger aliwataja wachezaji chipukizi watakaoingia kambini ni Tumaini Martin na Goodluck Shelemo kutoka Arusha, John Njau, Abuu Khamis, Brian Mallya na Salum Msafiri wa Dar es Salaam na Yassin Shabani aliyeko Nairobi, Kenya ambao wataungana na wachezaji wakongwe Hassan Kassim na Ommary Abdalla.

Katibu huyo alijivunia kikosi hicho ambacho kinaundwa na wachezaji wengi chipukizi kwamba kitaweka historia kwa Tanzania.

Inger aliwashukuru Tanga Cement kupitia Saruji chapa Simba kwa kukubali mwito wa TTA na kusaidia timu hiyo. Hiyo itakuwa ni mara ya kwanza katika historia Tanzania kuingia kwenye kinyang’anyiro cha Davis Cup.



Habari Leo

1 comment:

  1. Tumshukuru Tanga Cement Company kwa udhamini wao, tunaomba na makampuni mengine yaige mifano kama hii kudhamini michezo mbalimbali na kukuza vipaji vya wachezaji!

    ReplyDelete