BAADHI ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam(UDSM), wameendelea na mgomo wa kutoingia madarasani wakishinikiza kupatiwa fedha za kujikimu kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu(HESLB).
Wanafunzi hao kutoka kitengo cha Uhandisi na Teknolojia(CoET) na Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma(SJMC), jana walikusanyika katika jengo la utawala huku wakiimba nyimbo za kuhamasishana.
Wanafunzi hao walidai kuwa waliomba kupatiwa fedha hizo na wakaahidiwa jana zingetoka lakini waliopatiwa fedha hizo ni watu wa vitengo vingine.
Wakizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina yao kwa kuhofia kusimamishwa masomo, wanafunzi kutoka SJMC walisema walilazimika kugomea na mitihani ambayo ilikuwa ifanyike jana asubuhi chuoni hapo.
“Sisi unavyotuona hapa tunachotaka ni fedha zetu, kama chuo wameshakabidhiwa kwanini hawataki kutupa?
Tunaishi maisha ya taabu hatuna fedha za kununua hata chai, hiyo mitihani tutaifanyaje, leo tumeamua kwa pamoja kuacha mitihani yao” alisema mmoja wa wanafunzi hao.
Wanafunzi hao ambao walikuwa wamesimama katika mlango wa kuingia katika jengo hilo walikuwa wamezuia mtu kutoka au kuingia katika ofisi hiyo huku wakisema hawataondoka mpaka kieleweke.
Hata hivyo wakati wakiendelea na madai hayo kiliingia kikundi kingine cha wanafunzi hao wakiwa wamebeba matawi ya miti na fimbo, huku wakiimba ‘Al-Shaabab’ na kusisitiza kupatiwa fedha zao.
Habari leo
0 comments