Monday, April 9, 2012

Mjengwa: Je, Ni Nani Anayemfariji Msichana Huyu Wa Miaka 18 Aliyeondokewa Na Mpenzi Wake?


Ndugu zangu,

Ni kazi ngumu kuwa wakili kwa anayeonekana na jamii kuwa ni 'shetani'. Lakini, kwenye hili la kifo cha kusikitisha cha msanii Steven Kanumba kuna haja ya kukaa chini na kutafakari kwa bidii.

Kuna maswali pia ya kujiuliza juu ya msichana huyu wa miaka 18 ambaye sehemu kubwa ya jamii imeshamuhukumu kuwa ni muuaji. Kuna hata ambao hawalijui jina lake la kamili, bali, anajulikana kama ' Lulu'. Jina lake ni Elizabeth Michael.

Simulizi ya Lulu inaonyesha kuwa yeye na Kanumba walikuwa na mahusiano. Na wivu pia umeingia kwenye mahusiano yao. Hivyo basi, ugomvi na hatimaye kifo cha Kanumba.

Uchunguzi kamili haujakamilika. Na kama haujakamilika, basi, Lulu anabaki kuwa ni mtuhumiwa na si muhusika na kifo hicho. Kumwita Lulu muuaji ni kuharakisha kutoa hukumu isiyo ya haki. Pamoja na machungu yetu, lakini wanadamu tunapaswa kuwa na subira.

Na ukweli unabaki, kuwa Lulu ni mwanadamu kama wewe na mimi. Na kwa yote yaliyotokea, anabaki kuwa ameondokewa na mpenzi wake. Je, ni nani anayemfariji msichana huyu wa miaka 18 aliyeondokewa na mpenzi wake?


Maggid Mjengwa,
Dar es Salaam.
0788 111 765

No comments:

Post a Comment