Friday, August 17, 2012

MUFTI; KUMPINGA KADHI NI KUJIENGUA UISLAM

na Asha Bani

MUFTI Sheikh Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Issa Shaaban Simba, amewaonya Waislamu wanaopinga uteuzi wake wa Kadhi Mkuu, akisema asiyemtaka kadhi huyo amejiengua katika Uislamu.

Simba, amewataka wananchi kupuuza kundi la watu hao, na kwamba waumini hao watakuwa wamebakia kama Waislamu jina na mavazi.

Mufti alitoa kauli hiyo juzi wakati wa futari ya pamoja iliyoandaliwa nyumbani kwa Mwenyekiti wa Taasisi ya Kiislamu ya Imam Bukhary, Sheikh Khalifa Khamis, eneo la Magomeni jijini Dar es Salaam.

Alisema kuwa anashukuru kwa kupata pongezi kwa watu na taasisi mbalimbali baada ya uteuzi huo wa kadhi ambao alidai kwamba amekuwa akiupigania kwa takriban miaka 27 na hatimaye amefanikiwa.

Alifafanua kuwa ingawa watu wanapinga lakini ni yeye pekee ndiye anateuliwa na Waislamu wote, lakini mwenye wajibu na kushinikizwa na tume ya dini ili aweze kumteua Kadhi Mkuu ni Mufti.

Simba alisisitiza kuwa tayari amefanikiwa kufanya hivyo kwa kumteua mtu mwenye maadili yote na misingi ya dini.

“Mimi nasema hivi, huyu ndiye kadhi niliyemteua na nimezingatia vigezo vyote, sasa kwa ambaye anampinga ina maana kesi zake hazitosikilizwa na kadhi huyu, basi yeye si Muislamu na kwamba amebaki jina na mavazi pekee,” alisema Mufti.

Aidha, Mufti Simba alizungumzia suala la ushiriki wa sensa kwa Waislamu na kusema kuwa wanatakiwa kupuuza propaganda za kikundi kidogo kinachotaka kuwavuruga watu kwani sensa ina umuhimu kwa serikali katika kujua idadi ya watu ili waweze kuleta maendeleo nchini, hivyo kuwataka wajitokeze kwa wingi.

Naye Kadhi Mkuu, Abdalah Mnyasi, alisema ameupokea uteuzi huo kwa mikono miwili ingawa hapo awali hakuwa anafahamu lolote kuhusiana na hilo lakini akaahidi kutomsusia mtu kwani kufanya hivyo ni kumsusia Mwenyezi Mungu.

Alisema Waislamu kwa kufuata dini yao ni lazima kuhukumiana na ni wajibu wao kukubali kuhukumiana kwa kuwa hukumu yenyewe itakuwa inafanywa na watu wenye busara, hekima na elimu.

Mnyasi alisema kwa sasa tayari ofisi yake imeanza kufanya kazi na inapokea kesi nyingi sana zikiwamo za ndoa na mirathi ambazo zinaongoza na kuwataka wenye matatizo ya kimahakama kufika ili kuweza kupata usuluhishi katika ofisi yake.

Naye Sheikh Khalifa, alisema uteuzi wa kadhi umezingatia maadili, hivyo wanaopinga wapuuzwe.
“Kwa msingi huo ni jambo la aibu na kufedhehesha sana kuonekana watu wazima wenye akili timamu wanaitwa masheikh, wanasimama kidete huku wakitokwa jasho kuwashawishi waumini kususia sensa ya taifa ili kuikwamisha serikali kujua idadi kamili ya wananchi wake,” alisema.

No comments:

Post a Comment