Tuesday, September 11, 2012

Waziri: tunakabiliana na foleni Dar es Salaam

Na Andrew Chale

NAIBU Waziri wa Ujenzi, Gryson Lwenge  amesema serikali kwa kushirikiana na wakandarasi wa ndani na nje ya nchi watahakikisha wanakabiliana na tatizo la foleni jijini Dar es Salaam kwa kuimarisha miundo mbinu ya barabara.
 
Lwenge alisema hayo leo jijini Dar es Salaam, wakati wa ziara yake ya kukagua barabara ya Kigogo yenye kilometa 6.4 na ile ya Jet yenye umbali wa kilometa 10.
 
Alisema, Serikali itahakikisha inapambana na tatizo hilo kwa kuimarisha miundombinu yote ya barabara licha ya kukabiliwa na changamoto ya kifedha na wananchi kufungua kesi ya kupinga kubomolewa nyumba zao kupisha upanuzi huo.
 
Hata hivyo, alisema baadhi ya maeneo katika ujenzi wa barabara hizo, yamesimama kutokana na wananchi kufungua kesi.
 
Alisema, barabara hiyo ya Jet yenye kilometa 10 itagharimu zaidi ya shilingi bil. 12.
 
Ziara hiyo itaendelea tena kesho katika daraja la Kigamboni, barabara ya Kilwa, mradi wa mabasi yaendayo kasi na barabara ya Mwenge na Tegeta.

No comments:

Post a Comment