SHIRIKISHO la mpira wa kikapu Tanzania (TBF) bado lipo katika hali ngumu ya kuandaa mashindano ya klabu bingwa kanda ya tano (Zone five) yatakayoanza mapema mwezi ujao kutokana na kukosa udhamini ila wanaendelea kufanya mazungumzo na baadhi ya makampuni yaliyoonyesha nia ya kusaidia.
Mashindano hayo yamepangwa kuanza Oktoba 9 hadi 18 jijini Dar es salam, ambapo Tanzania itawakilishwa na timu sita zikiwamo tatu za wanaume na tatu za wanawake.
Katibu msaidizi wa TBF, Michael Maluwe alisema hivi sasa wako katika maandalizi ya kusaka wadhamini na wanaendelea na mazungumzo na makampuni ambayo yameonyesha nia ya kutoa msaada.
Alisema mpaka sasa takribani nchi nane tayari zimethibitisha ushiriki wake ambazo ni pamoja na Kenya timu 4, Uganga 4, Rwanda 4, Burundi 4, Ethiopia 1 ya wanawake na Somalia itawakilishwa na timu 1.
Maluwe alisema Tanzania timu itawakilishwa na timu za wanawake ambazo ni Jeshi Stars, Lady Lions pamoja na Magereza na timu za wanaume ambazo ni Savio, ABC na Vijana zote za Jijini Dar es salaam.
"Hatuwezi kuhairisha mashindano haya kwani tayari tumethibitisha kuwa wenyeji na kuyaandaa, kikubwa kwa sasa tunakimbizana na wadhamini ili waweze kutusaidia kufanikisha mashindano haya ambayo ni makubwa na yenye kuhitaji maandalizi ya kutosha,"alisema Maluwe.
Aidha aliongeza kuwa taari timu za Tanzania zimeanza maandalizi yake kwa kufanya mazoezi kila jioni kwenye uwanja wa ndani wa Taifa pamoja na uwanja wa Mgulani kwa ajili ya kujiandaa na mashindano hayo.
Mwananchi.co.tz



0 comments