na Gordon Kalulunga, Mbeya
WANAFUNZI 33 wa Chuo cha Ilemi Polytechnic College cha mkoani hapa, wanadaiwa kufuja sh milioni 12, 450,000 za ada ambazo walipaswa kulipa kwa ajili ya mafunzo.
Wanachuo hao badala ya kulipa ada hizo katika akaunti ya chuo katika Benki ya Exim, walikuwa wakichukua stakabadhi ya malipo na kuzigonga muhuri bandia, kisha kuzipeleka kwa mhasibu wa chuo hicho kuthibitisha kuwa walikuwa wamelipa ada.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, umebaini kuwa kati ya wanafunzi hao, wa kike pekee baada ya kubanwa na uongozi wa benki na chuo ndipo waliweza kukiri kufanya udanganyifu huo.
Hata hivyo, katika udanganyifu huo, benki hiyo ilisema haijapata hasara yoyote, na kwamba wanafunzi hao pekee ndio wameathirika kwa asilimia kubwa kutokana na kudaiwa ada hizo.
Mkuu wa chuo hicho, Bon Mwasaka, alisema kuwa wanachuo waliofanya udanganyifu huo ni wale waliojiunga na masomo kwa mwaka wa kwanza.
Alisema kuwa chuo chake hakijapata hasara yoyote kwani baada ya kuwabaini, watalazimika kulipa upya huku uchunguzi ukiendelea kufanyika ili kubaini mtandao huo.
Meneja wa Benki ya Exim, Godfrey Kitundu, alisema wamebaini kasoro zaidi ya 14 za muhuri huo, ambazo zimeonekana, hivyo haikuwa rahisi benki hiyo kudanganywa na nyaraka hizo za kughushi.
Chuo hicho hutoa mafunzo ya kilimo, biashara na kompyuta (ICT) kwa gharama ya sh 700,000, ambazo ni gharama za kila mwanachuo mmoja kwa hatua ya cheti na diploma.
0 comments