Thursday, January 12, 2012

Mtihani kidato cha II wapandishwa hadhi

Halima Mlacha

SERIKALI imetangaza rasmi kuupa hadhi mtihani wa taifa wa kidato cha pili na kuanzia mwaka huu, mwanafunzi atakayepata chini ya wastani wa asilimia 30, hataendelea na kidato cha tatu na atalazimika kukariri kidato cha pili.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, alisema uamuzi wa Serikali umetokana na uchunguzi uliofanywa na Tume iliyoundwa na Serikali kutafiti chanzo cha kufeli kwa wanafunzi wa kidato cha nne mwaka juzi.

“Naomba ieleweke, kwamba mfumo huo haukufutwa kabisa ila mwaka 2008 Serikali ilitamka kuwa wanafunzi ambao watakosa alama ya asilimia 30 katika mtihani wa kidato cha pili, hawatakariri darasa kama miaka ya nyuma, ila wataendelea na masomo ya kidato cha tatu,” alisema Mulugo.

Hata hivyo, alisema uchunguzi wa mwaka jana, kuhusu ufaulu duni wa wanafunzi katika mtihani wa kidato cha nne mwaka juzi, ulibaini kuwa moja ya sababu za wanafunzi hao kufanya vibaya ni kuwaruhusu kuendelea na masomo baada ya kushindwa kufikia alama stahiki katika mtihani wa kidato cha pili.

Aidha, alisema takwimu zinaonesha kuwa ufaulu wa mtihani wa kidato cha pili umekuwa ukishuka mwaka hadi mwaka, kuanzia mwaka 2008 hadi mwaka juzi, hivyo kuashiria kuwa wanafunzi na walimu hawafanyi bidii za makusudi kujifunza na kufundisha.

Alisema ufaulu wa wanafunzi katika mtihani huo mwaka 2008 ulikuwa asilimia 73, mwaka 2009 asilimia 69.3 na 2010 asilimia 61.9.

Mulugo alisema kutokana na hali hiyo, kuanzia mwaka huu mwanafunzi atakayepata chini ya wastani wa asilimia 30 atarudia darasa mara moja, akifeli tena mwaka mwingine atafutwa kabisa katika mfumo wa elimu nchini.

0 comments