ZAIDI ya abiria 30, wameteketea kwa moto baada ya basi la kampuni ya Dilux Coach walilokuwa wakisafiria kupinduka na kuwaka moto.
Ajali hiyo ya kusikitisha, ilitokea jana majira ya saa tisa jioni katika eneo la Misugusugu, wilaya ya Kibaha mkoani Pwani.
Basi hilo lenye namba za usajili T344 AAT aina ya Volvo, lilikuwa likitokea Dar es Salaam kwenda mkoani Dodoma, lakini lilipofika katika eneo hilo tairi la mbele, upande wa kulia lilipasuka na kupinduka kisha kuwaka moto.
Tanzania Daima ambalo lilifika eneo la tukio, lilishuhudia miili ya abiria zaidi ya 30 ikiteketea kabisa na kubaki majivu na kuwa vigumu kuitambua.
Abiria waliojeruhiwa katika ajali hiyo, walikimbizwa katika hospitali ya Tumbi, Kibaha kwa matibabu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ernest Mangu, alisema kuwa abiria 17 pekee ndio waliotoka salama katika gari hilo wakiwa wamejeruhiwa baada ya kuhangaika na kupata nafasi ya kutoka mara baada ya moto kuanza kuteketeza basi hilo.
Hata hivyo dereva wa gari hilo haijajulikana kama amepona au la na taarifa kutoka kwa vyanzo tofauti ambazo hazijathibitishwa na polisi, zilidai kuwa gari hilo lilitoka katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Ubungo likiwa na abiria 42 na kati yao 17 tu, ndio walionusurika.
Mashuhuda wa ajali hiyo walisema kuwa baada ya gari hilo kuanza kuwaka moto walijaribu kutafuta njia ya haraka ya kuuzima bila mafanikio na hata gari la zima moto lilipofika, tayari abiria walioshindwa kutoka walikuwa wameshateketea na kubaki majivu.
Kamanda Mangu alikemea tabia ya mwendo kasi kwa baadhi ya madereva ambayo kwa asilimia kubwa ndiyo chanzo cha ajali nyingi za barabarani.
Kamanada Mangu, alisema watafanya uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha ajali hiyo pamoja na kufuatilia idadi kamili ya abiria waliokuwapo ndani ya basi hilo wakati likitoka Ubungo.
Hali katika viwanja vya Hospitali ya Tumbi, Kibaha ambako ndugu wa majeruhi hao walifika kuwajulia hali, ilitawaliwa na vilio na simanzi kubwa. Katika hali isiyo ya kawaida, licha ya chumba cha maiti kuandaliwa kupokea miili ya waliopoteza maisha katika ajali hiyo, hakuna hata maiti moja iliyopatikana kwani wote waliteketea na kubaki majivu.
Tanzania Daima
0 comments