Thursday, October 27, 2011

China watoa msaada wa vifaa vya michezo

SERIKALI ya China imetoa msaada wa vifaa mbalimbali vya michezo ikiwa ni pamoja na mipira 300 kwa Wizara ya Habari,Vijana Utamaduni na Michezo ikiwa ni sehemu ya kuboresha uhusiano kati ya Serikali ya Tanzania na nchi hiyo.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya vifaa hivyo Balozi wa China nchini Liu Kinsheng alisema licha ya kutoa mipira ya miguu, Serikali yake pia imetoa zaidi ya baiskeli 15 ambazo zitakwenda katika jimbo la Dr. Nchimbi pamoja na vifaa vya michezo ya kichina vitakavyokwenda katika chama cha michezo ya Kichina Tanzania (WUSHU).

Akipokea msaada wa vifaa hivyo jijini Dar es Salaam, Dk. Nchimbi alisema kuwa wengi wanahisi kuwa mpira wa miguu tu unapewa kipaumbele kwa misaada, tofauti na vyama vya michezo mingine kama vile ngumi na riadha ambazo pia vinahitaji msaada wa kifedha na vifaa.

Alisema wanamichizo ni sehemu ya Jumuia za Vijana ambao kama Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inawajibu wa kusaidia kila inapowezekana ili kurudisha maendeleo ya michezo nchini.

Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Michezo ya Kichina Tanzania (WUSHU), Fred Maiga alisema vitasaidia kuendeleza mchezo wa kichina wa simba na nyoka kwa vijana wa Kitanzania ambao mchezo huo umekuwa ukidorora siku hadi siku.

“Tunaishukuru Serikali ya China kwa msaada wa vifaa vya mchezo wa nyoka na simba kwani michezo hii imekuwa ikidorora siku hadi siku hivyo kwa msaada huu itaimarisha kwa kasi ukuaji wa michezo ya Kichina na hatimaye tutakuwa na nafasi ya kuingiza timu katika mashindano ya olimpiki,” alisema.



Habari leo

0 comments