WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee amesema kwamba Serikali haina ubaguzi katika kuwapatia mikopo ya Elimu ya Juu wanafunzi wa Zanzibar.
Akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakati wa kuchangia hoja binafsi iliyowakilishwa na mwakilishi Hamza Hassan Juma, Mzee alisema, Serikali haina ubaguzi katika kuwasomesha vijana wake ila tatizo inakabiliwa na uhaba wa fedha.
Alisema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tangu baada ya Mapinduzi ilikuwa na azma hiyo kwa kuwasomesha wanafunzi wote bure, azma ambayo bado ipo hadi leo.
Alisema, Serikali inakabiliwa na uhaba wa bajeti yake katika masuala mbalimbali ambapo mambo mengi yanayotakiwa kutekelezwa katika miradi iliyotengwa ni muhimu kwa maisha ya binadamu.
Akifafanua, alisema katika bajeti ya mwaka huu zimetengwa Sh bilioni 15.3 kwa ajili ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, lakini zilizopatikana ni Sh bilioni nne tu.
“Tunakabiliwa na tatizo la ukosefu wa fedha katika bajeti yetu ambayo tumetenga kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo...kwa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu tumetenga Sh bilioni 15.3 tumewapa Sh bilioni nne tu...huo ndiyo uwezo wetu katika kuhudumia wanafunzi,” alisema.
Hata hivyo, aliwakumbusha wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwamba muswada wa kuanzishwa kwa Bodi ya mikopo ya elimu ya juu wameupitisha wao ambao unawataka watu waliokopa kurudisha fedha hizo.
Alisema, Sh bilioni saba hazijarejeshwa kwa wanafunzi waliochukua mikopo hiyo ambao tayari baadhi yao wameanza kufanya kazi katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
“Tatizo letu moja kubwa ni kwamba tunatunga sheria, lakini hatuzitekelezi...wanafunzi waliochukua mikopo wanadaiwa zaidi ya Sh bilioni saba sasa, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa,” alisema.
Habari leo
0 comments