Friday, October 28, 2011

Kuharibu sim-card faini mil 30

BARAZA la ushauri la watumiaji wa huduma za mawasiliano Tanzania (TCRA-CCC) limetoa onyo kali kwa watumiaji wa simu za mikononi ambao watabainika kuharibu kusudi simu zao za mikononi sim- card (mfano kuflash ) kuwa adhabu yake ni faini ya shilingi milioni 30 au kifungo jela kisichozidi miaka 10.

Akizungumza kwa nyakati tofauti na wanahabari mkoani Iringa jana na wanafunzi wa shule ya sekondari ya Lugalo katika warsha ya siku moja, Ofisa Mwandamizi Elimu na Uhamasishaji wa baraza hilo, Mary Msuya, alisema idadi kubwa ya watumiaji wa huduma mbalimbali za mawasiliano wamekuwa wakivunja sheria bila kujua.

Aliainisha makosa mengine na adhabu zake kuwa ni pamoja na kutumia sim card bila kusajiliwa kosa ambalo adhabu yake ni faini isiyozidi sh 500,000 au kifungo kisichozidi miezi mitatu, na kushindwa kuripoti wizi au upotevu adhabu ni faini ya sh 300,000 hadi sh 500,000 au kifungo cha miezi sita, ama vyote kwa pamoja.

Aidha, alisema kuharibifu wa miundombinu ya posta na mawasiliano ya kielektroniki adhabu yake ni faini isiyozidi sh millioni moja au kifungo kisichopungua miaka mitatu jela, au vyote kwa pamoja.

Kwa upande mwingine, alisema watumiaji wana haki ya msingi ya kibinadamu ya kupata taarifa za mawasiliano kwa bei halali hasa huduma za msingi kama simu, posta na utangazaji bila kubabaishwa.



Tanzania daima

0 comments