KANISA Katoliki nchini (TEC) limeshitushwa na kutishwa na hatua ya Rais Jakaya Kikwete kusaini Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011, harakaharaka kwa kuwa kunaweza kuipeleka nchi pabaya.
Akizungumza juzi jijini Mwanza na Tanzania Daima muda mfupi baada ya kumalizika kwa hafla ya uzinduzi wa Kitabu cha Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara, kilichoandikwa na John Kasembo, Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania, Jude Thadeus Ruwa'ichi, alisema Watanzania wengi walitaka muswada huo usisainiwe, na kwamba mkuu huyo wa nchi alipaswa kusikiliza mawazo ya wananchi wake, na si kuwahi kusaini na kuwa sheria.
Rais huyo wa TEC alisema kitendo cha serikali kukusanya maoni katika mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam na Zanzibar peke yake, haitoshi kujenga hoja ya kusaini ama kupitisha muswada huo wa Katiba.
Ruwa'ichi alisema suala la kuundwa kwa Katiba mpya si hiari ya rais wala kundi na tabaka fulani, bali ni la Watanzania wote.
Rais huyo wa TEC ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza alisema hatua ya kulipeleka suala la Katiba mbindembinde linaweza kuipeleka nchi kubaya na Kanisa Katoliki halitaki Watanzania wafike huko.
Alisema walitegemea Kikwete angethamini na kujali maoni ya wadau wengine, lakini katika namna ya ajabu hakuonekana kujali chochote.
Ruwa'ichi ambaye alikuwa miongoni mwa wageni waalikwa katika uzinduzi wa kitabu hicho, alieleza kushangazwa na kitendo cha Bunge kupitisha harakaharaka muswada huo.
"Hivi Bunge linashughulikia masilahi ya nani? Wabunge wamepewa dhamana na wananchi, hivyo ni lazima wawasikilize wanachotaka, halafu ndicho wakifanyie kazi, na si kuonekana kama ushabiki fulani".
Alipoulizwa kuhusu suala la udini linaloonekana kutumiwa na baadhi ya wanasiasa nchini, Rais huyo wa Baraza la Maaskofu alikiri kuwapo kwa jinamizi hilo, na kusema ajenda ya udini kwa sasa imekuwa kama kichaka cha watu fulani kuficha maovu yao.
Alionya kwamba iwapo serikali itaruhusu mijadala ya udini kutawala nchini, basi taifa lipo hatarini kupoteza ustawi wake, na akataka watu wasitumie mgongo wa dini kuficha madhambi yao.
Tanzania Daima
0 comments